villafm

INEC YAWANOA WASIMAMIZI WA VITUO VYA UCHAGUZI JIMBO LA KWAHANI

  • Home    /
  • INEC YAWANOA WASIMAMIZI WA VITUO VYA UCHAGUZI JIMBO LA KWAHANI
INEC YAWANOA WASIMAMIZI WA VITUO VYA UCHAGUZI JIMBO LA KWAHANI

Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya Kupiga Kura Jimbo la Kwahani Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar wametakiwa kufanya kazi kwa kujiamini, uadilifu na weledi wanapotekeleza majukumu yao ya uchaguzi kutokana na dhamana waliyopewa na Tume. Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dkt.Zakia Mohamed Abubakar wakati akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya vituo yanayofanyika kuanzia leo tarehe 5 hadi 6 Juni, 2024 Skuli ya Sekondari ya Lumumba, Mjini Magharibi- Zanzibar. “Mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu ya Imani ya Tume kuwa mnao uwezo wa kufanya kazi hii, Jambo muhimu mnalotakiwa kulizingatia ni kujiamini na kufanya kazi kwa weledi, na kwamba katika utendaji wa majukumu yenu mnapaswa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake, Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume,”alisema Mh. Dkt. Zakia. Mhe. Dkt Zakia amesema, kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hii ni pamoja na Chaguzi ndogo zinazojitokeza kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo vifo kama ilivyotokea katika Jimbo la Kwahani. “Hata hivyo, pamoja na kuwa Tume ndiyo yenye jukumu hilo, wanaoratibu na kusimamia Uchaguzi ngazi ya Vituo ni nyinyi tuliowateua pamoja na watendaji wengine”. Aidha, Mhe. Dkt Zakia amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa na kuzingatiwa kwani hatua na taratibu hizo ndio msingi wa Uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondosha kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa Uchaguzi. Amewataka washiriki hao wa mafunzo kuwa watulivu na kupokea mada zitakazowasilishwa, wabadilishane uzoefu na kujadili namna ya kufanikisha Uchaguzi katika Jimbo la Kwahani.

leave a comment

0 comments

login

author_img

Copyright © 2024 Villa Fm Developed by Villa Fm.

Adonis Music R&B